Katika mkutano wetu wa mwisho tuliweza kuzungumzia mada muhimu sana. Je, mnakumbuka mada hiyo ilikuwa kuhusu nini? Hebu Niirudie. Mada ya ushirika wetu wa mwisho ilikuwa: Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe. Je, mada hii ni muhimu kwenu? Ni sehemu gani katika mada hii ni muhimu kwenu? Kazi ya Mungu, tabia ya Mungu, au Mungu Mwenyewe? Ni sehemu ipi inawavutia zaidi? Ni sehemu ipi mnayotaka kusikiliza kuhusu zaidi? Najua ni vigumu kwenu ninyi kulijibu swali hilo, kwa sababu tabia ya Mungu inaweza kuonekana katika kila kipengele cha kazi Yake, na tabia Yake inafichuliwa katika kazi Yake siku zote na pahali pote, na, kutokana na hayo, inawakilisha Mungu Mwenyewe; kwenye mpango wa usimamizi wa ujumla wa Mungu, kazi ya Mungu, tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe vyote hivi haviwezi kutenganishwa.
Maudhui ya ushirika wetu wa mwisho kuhusu kazi ya Mungu yaliweza kuangazia mambo yaliyofanyika kitambo kwenye Bibilia. Maudhui hayo yote yalikuwa hadithi kuhusu binadamu na Mungu, na yalimfanyikia binadamu na wakati huohuo yakahusisha kushiriki na maonyesho ya Mungu, hivyo basi hadithi hizi zinashikilia thamani na umuhimu mkubwa katika kujua Mungu. Baada tu ya kuumba binadamu, Mungu Alianza kujihusisha na binadamu na kuzungumza na binadamu, na tabia yake ikaanza kuonyeshwa kwa binadamu. Kwa maneno mengine, tangu Mungu alipojihusisha kwanza na wanadamu, Alianza kuweka wazi kwa mwanadamu, bila kusita, kiini Chake halisi na kile Anacho na alicho. Licha ya kama watu wa awali au watu wa leo wanaweza kuona au kuelewa kiini hicho, kwa ufupi Mungu anamzungumzia mwanadamu na kufanya kazi miongoni mwa binadamu, Akifichua tabia Yake na Akionyesha kiini Chake—jambo ambalo ni ukweli, na lisilopingika na mtu yeyote. Hii inamaanisha pia kwamba tabia ya Mungu, kiini cha Mungu, na kile Anacho na alicho vyote vinatolewa daima na kufichuliwa huku naye Akifanya kazi na kujihusisha na binadamu. Hajawahi kusetiri au kumfichia binadamu chochote, lakini badala yake anatangaza kwa umma na kuachilia tabia Yake binafsi bila ya kuficha chochote. Hivyo basi, Mungu anatumai kwamba binadamu anaweza kumjua Yeye na kuielewa tabia Yake na kiini chake. Hapendi binadamu kuchukulia tabia Yake na kiini Chake kuwa mafumbo ya milele, wala Hataki wanadamu kumchukulia Mungu kama fumbo lisiloweza kutatuliwa. Mpaka tu pale ambapo wanadamu watakapomjua Mungu ndipo binadamu atakapojua njia ya kufuata na kuweza kuukubali mwongozo wa Mungu, na wanadamu tu kama hawa ndio wanaoweza kuishi kwa kweli katika utawala wa Mungu, na kuishi katika mwangaza, na kuishi katikati ya baraka za Mungu.
Maneno na tabia iliyowasilishwa mbele na kufichuliwa na Mungu inawakilisha mapenzi Yake, na pia inawakilisha kiini Chake halisi. Wakati Mungu anapojihusisha na binadamu, haijalishi ni nini Anachosema au kufanya, au tabia gani Anayofichua, na haijalishi ni nini binadamu anaona kuhusu kiini cha Mungu na kile Anacho na alicho, vyote vinawasilisha mapenzi ya Mungu kwa binadamu. Licha ya kiwango ambacho binadamu anaweza kutambua, kufahamu, au kuelewa, vyote hivi vinawakilisha mapenzi ya Mungu—mapenzi ya Mungu kwa binadamu. Hili ni bila shaka! Mapenzi ya Mungu kwa binadamu ni vile Anavyohitaji watu kuwa, kile Anachohitaji wao kufanya, namna Anavyohitaji wao kuishi, na vile Anavyowahitaji kuweza kukamilisha kutimia kwa mapenzi ya Mungu. Je, mambo haya hayawezi kutenganishwa na kiini cha Mungu? Kwa maneno mengine, Mungu huwasilisha mbele tabia Yake na chote Alicho nacho na alicho wakati huohuo Akimtolea madai binadamu. Hakuna uongo, hakuna kusingizia, hakuna ufichaji, na wala hakuna kupiga chuku. Ilhali kwa nini binadamu hawezi kujua na kwa nini hajawahi kuweza kutambua waziwazi tabia ya Mungu? Na kwa nini hajawahi kutambua mapenzi ya Mungu? Kile ambacho kimefichuliwa na kuwasilishwa mbele na Mungu ndicho kile Mungu anacho Mwenyewe na maana yake, na kinaonyesha kila kipengele cha tabia Yake ya kweli—hivyo kwa nini binadamu hawezi kuona? Kwa nini binadamu hana uwezo wa kuwa na maarifa ya kina? Kunayo sababu muhimu ya haya. Na sababu yenyewe ni ipi? Tangu wakati wa uumbaji, binadamu hajawahi kumchukulia Mungu kama Mungu. Kwenye nyakati zile za mwanzo kabisa, haikujalisha ni nini Mungu alifanya kuhusiana na binadamu, yule binadamu ambaye ndiye tu alikuwa ameumbwa, binadamu alimchukulia yeye kuwa mwandani wake tu na wala si zaidi ya hapo, kama mtu wa kutegemewa, na hakuwa na maarifa yoyote wala uelewa wa Mungu. Hivi ni kusema, hakujua kwamba kile kilichowasilishwa mbele na Kiumbe huyu—Kiumbe huyu ambaye yeye alitegemea na kumwona kuwa mwandani wake—alikuwa kiini cha Mungu, na wala hakujua kwamba Kiumbe huyu ndiye anayetawala viumbe wote. Nikisema kwa urahisi, watu wa wakati huo hawakuwa na maarifa hata kidogo kumhusu Mungu. Hawakujua kwamba mbingu na nchi na mambo yote yalikuwa yameumbwa na Yeye na wala hawakujua ni wapi Alipotokea, na, zaidi hawakujua Yeye Alikuwa nani. Bila shaka, wakati huo Mungu hakumhitaji binadamu kumjua Yeye au kumfahamu Yeye au kuelewa kila kitu Alichofanya, au kufahamishwa kuhusu mapenzi Yake, kwani hizi zilikuwa nyakati za mapema zaidi baada ya uumbwaji wa wanadamu. Wakati Mungu alipoanza matayarisho ya kazi ya Enzi ya Sheria, Mungu alifanya mambo fulani kwa binadamu na pia Akaanza kutolea binadamu madai fulani, Akimwambia namna ya kutolea Mungu sadaka na namna ya kumwabudu. Ni wakati huo ndipo binadamu alipopata mawazo machache mepesi kuhusu Mungu, ni hapo tu ndipo alipojua tofauti kati ya binadamu na Mungu na kwamba Mungu Ndiye aliyewaumba wanadamu. Wakati binadamu alipojua kwamba Mungu alikuwa Mungu na binadamu alikuwa binadamu kukawa umbali fulani kati ya Yeye na Mungu, bado Mungu hakuhitaji kwamba binadamu awe na maarifa makuu au uelewa wa kina kumhusu Yeye. Hivyo basi, Mungu anayatoa mahitaji tofauti kwa binadamu kutokana na awamu na hali za kazi Yake. Mnaona nini katika haya? Ni kipengele kipi cha tabia ya Mungu unayoitambua? Je, Mungu ni wa kweli? Yale mahitaji ambayo Mungu anampa binadamu yanastahili? Kwenye nyakati za mapema kabisa kufuatia uumbaji wa wanadamu na Mungu, wakati ambao Mungu alikuwa bado hajatekeleza kazi ya ushindi na utimilifu wa binadamu, na Alikuwa hata bado hajaongea yale maneno mengi sana kwake, Alihitaji kidogo sana kutoka kwa binadamu. Licha ya kile ambacho binadamu alifanya na namna alivyotenda—hata kama alifanya mambo fulani yaliyomkosea Mungu—Mungu alimsamehe hayo yote, na akayapuuza. Kwa sababu Mungu Alijua kile Alichokuwa Amempa binadamu, na Alijua kile kilichokuwa ndani ya binadamu, basi Alijua kiwango cha mahitaji ambayo anafaa kudai kutoka kwa binadamu. Ingawaje kiwango cha mahitaji Yake kilikuwa cha chini sana wakati huo, hii haimaanishi kwamba tabia Yake haikuwa kuu, au kwamba hekima na uweza Wake yalikuwa si yoyote ila maneno matupu. Kwa binadamu, kunayo njia moja tu ya kujua tabia ya Mungu na Mungu Mwenyewe: kwa kufuata hatua za kazi ya usimamizi ya Mungu na wokovu wa wanadamu, na kuyakubali maneno ambayo Mungu anaongea akiyaelekeza kwa wanadamu. Kujua kile Mungu anacho na alicho, na kujua tabia ya Mungu, bado binadamu angemuuliza Mungu kumwonyesha nafsi Yake halisi? Binadamu hatafanya hivyo, na hathubutu kufanya hivyo, kwa kuweza kuifahamu tabia ya Mungu na kile Anacho na alicho, tayari binadamu atakuwa amemwona Mungu Mwenyewe wa kweli, na atakuwa tayari ameona nafsi Yake halisi. Haya ndiyo matokeo yasiyoepukika.
Kazi na mpango wa Mungu ulipokuwa ukiendelea mbele bila kusia, na baada ya Mungu kuanzisha agano la upinde wa mvua na binadamu kama ishara kwamba Hangewahi tena kuuangamiza ulimwengu kwa kutumia gharika, Mungu alikuwa na tamanio lililokuwa likiongezeka na kumsukuma kuwapata wale ambao wangeweza kuwa katika akili moja na Yeye. Hivyo, pia, Alikuwa na tamanio la haraka zaidi la kupata wale waliokuwa na uwezo wa kufanya mapenzi Yake duniani, na, isitoshe, kupata kundi la watu ambao wangeweza kuwa huru dhidi ya nguvu za giza, na kutoweza kuwa watumwa wa Shetani, na kuweza kuwa na ushuhuda kwake Yeye duniani. Kupata kundi la watu kama hawa kulikuwa ni tamanio la Mungu kwa muda mrefu, Alichokuwa akisubiria tangu wakati wa uumbaji. Hivyo basi, licha ya matumizi ya gharika na Mungu ili kuuangamiza ulimwengu, au agano Lake na binadamu, mapenzi ya Mungu, hali yake ya akili, mpango, na matumaini yote yalibakia yaleyale. Kile Alichotaka kufanya, ambacho Alikuwa ametamani kwa muda mrefu kabla ya uumbaji, kilikuwa kupata wale walio miongoni mwa wanadamu ambao Alitamani kuwapata—Kupata watu wa kundi hili ambao walioweza kufahamu na kujua tabia Yake, na kuyaelewa mapenzi Yake, kundi ambalo lingeweza kumwabudu Yeye. Watu kwenye kundi kama hili wanaweza kweli kuwa na ushuhuda kwake, na wao ndio, yaweza kusemekana, wasiri Wake.
Leo, hebu tuendelee kuzifuata nyayo za Mungu na kufuata nyayo za kazi Yake, ili tuweze kufichua fikira na mawazo ya Mungu, na kila kitu kinachomhusu Mungu, vyote ambavyo "vimehifadhiwa kwenye ghala" kwa muda mrefu. Kupitia mambo haya tutajua hatimaye tabia ya Mungu, kukielewa kiini cha Mungu, tutamruhusu Mungu kuingia kwenye mioyo yetu, na kila mmoja wetu ataweza kukaribia Mungu kwa utaratibu, na kupunguza umbali wetu na Mungu.
Sehemu ya kile tulichozungumzia wakati wa mwisho ilihusiana na kwa nini Mungu alianzisha agano na binadamu. Wakati huu, tutakuwa na ushirika kuhusu vifungo vya maandiko vilivyo hapa chini. Hebu tuanze kwa kuyasoma maandiko.
A. Ibrahimu
1. Mungu Amwahidi Ibrahimu Mwana
Mwa 17:15-17 Naye Mungu akasema kwake Ibrahimu, na kuhusu Sarai mke wako, hutamwita kwa jina lake la Sarai, kwa maana sara ndilo litakuwa jina lake. Na mimi nitambariki yeye, na pia nitakupa mwana kutoka kwake: ndiyo, nitambariki yeye, na yeye atakuwa mama yao mataifa; wafalme wa watu watatoka kwa yeye. Kisha Ibrahimu akaanguka chini kifudifudi, na kucheka, na akasema moyoni, Je, mtoto atazaliwa kwa mtu mwenye umri wa miaka mia moja? naye Sara, aliye na umri wa miaka tisini, atazaa?
Mwa 17:21-22 Lakini nitaliimarisha agano langu na Isaka, ambaye Sara atakuzalia wewe wakati kama huu mwaka ujao. Naye akakoma kuzungumza na yeye, na Mungu akapanda juu kutoka kwa Ibrahimu.
2. Ibrahimu Amtoa Isaka
Mwa 22:2-3 Naye akasema, Umchukue mwana wako sasa, mwana wako wa pekee Isaka, unayempenda, na uende hadi nchi ya Moria; na huko umtoe kwa sadaka ya kuteketezwa juu ya mojawapo ya milima ambayo nitakuambia. Naye Ibrahimu akaamka asubuhi mapema, na kuweka tandiko kwa punda wake, akawachukua vijana wake wawili pamoja naye, naye Isaka mwana wake, na akapasua kuni kwa sababu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, na akaondoka, na kuenda pahali ambapo alikuwa ameambiwa na Mungu.
Mwa 22:9-10 Na wakafika pahali hapo ambapo Mungu alikuwa amemwambia; naye Ibrahimu akajenga madhabahu hapo, na kuziweka kuni kwa mpango, na kumfunga Isaka mwana wake, naye akamlaza juu ya madhabahu kwa zile kuni. Na Ibrahimu akanyosha mbele mkono wake, na kukichukua kisu ili amchinje mwana wake.
Hakuna Awezaye Kuzuia Kazi Ambayo Mungu Anaamua Kufanya
Hivyo, muda mfupi uliopita nyote mmesikia hadithi ya Ibrahimu. Alichaguliwa na Mungu baada ya gharika kuuangamiza ulimwengu, jina lake lilikuwa Ibrahimu, na alipokuwa na miaka mia moja, na mke wake Sara akiwa na umri wa miaka tisini, ahadi ya Mungu ilimjia. Mungu alimwahidi nini? Mungu alimwahidi kile ambacho kinarejelewa katika Maandiko: "Na mimi nitambariki yeye, na pia nitakupa mwana kutoka kwake." Ni maelezo yapi yalitangulia ahadi ya Mungu ya kumpa mtoto? Maandiko yanaelezea yafuatayo: "Kisha Ibrahimu akaanguka chini kifudifudi, na kucheka, na akasema moyoni, Je, mtoto atazaliwa kwa mtu mwenye umri wa miaka mia moja? naye Sara, aliye na umri wa miaka tisini, atazaa?" Kwa maneno mengine wanandoa hawa wazee walikuwa na umri mwingi sana wa kupata watoto. Naye Ibrahimu alifanya nini baada ya Mungu Kumwahidi? Aliuangukia uso wake akicheka, na kujiambia, "Je, mtoto atazaliwa kwa mtu mwenye umri wa miaka mia moja?" Ibrahimu aliamini kwamba haikuwezekana—hivi alimaanisha kwamba alisadiki ahadi ya Mungu kwake haikuwa chochote ila mzaha. Kutoka mtazamo wa binadamu, ahadi isingeweza kutimizika na binadamu, na vilevile isingeweza kutimizika na Mungu na ilikuwa haiwezekani kwa Mungu. Pengine, kwa Ibrahimu, ahadi hii ilikuwa ya kuchekesha. Mungu alimuumba binadamu, lakini yaonekana kwamba hajui kwamba mtu aliyezeeka sana hawezi kupata watoto; Anafikiria kwamba Anaweza kuniruhusu
kupata mtoto, Anasema kwamba atanipa mtoto—kwa kweli hilo haliwezekani! Na hivyo, Ibrahimu akaangukia uso wake na kucheka, akijifikiria yeye mwenyewe: Haiwezekani—Mungu anafanya mzaha na mimi, hili haliwezi kuwa kweli. Hakutilia maanani maneno yake Mungu. Hivyo, katika macho ya Mungu, Ibrahimu alikuwa binadamu wa aina gani? (Mwenye haki) Ni wapi ulipojifunza kwamba alikuwa mwenye haki? Ninyi mnafikiria kwamba wale wote ambao Mungu anawaita ni wenye haki, na watimilifu, na watu wanaotembea na Mungu. Wewe unashikilia mafundisho ya dini! Lazima uone waziwazi kwamba wakati Mungu anapomfasili mtu, Hafanyi hivyo kiholela. Hapa, Mungu hakusema kwamba Ibrahimu alikuwa mwenye haki. Katika moyo Wake, Mungu anavyo viwango vya kupima kila mtu. Ingawaje Mungu hakusema ni mtu wa aina gani ambaye Ibrahimu alikuwa, kwa mujibu wa mwenendo wake, Ibrahimu alikuwa na imani ya aina gani kwake Mungu? Ilikuwa ya kidhahania kidogo? Au alikuwa mwenye imani kuu? La, hakuwa! Kicheko na fikira zake zilionyesha yeye alikuwa nani, hivyo imani yenu kwamba alikuwa mwenye haki ni ndoto ya kufikiria kwenu, ni matumizi yasiyo na mwelekeo ya mafundisho ya dini, usiopaswa. Je, Mungu alikiona kicheko cha Ibrahimu na maonyesho yake madogo, Alijua kuyahusu? Mungu alijua. Lakini Mungu angebadilisha kile Alichokuwa ameamua kufanya? La! Wakati Mungu alipopangilia na kuamua kwamba Angemchagua binadamu huyu, suala hilo lilikuwa tayari limekamilishwa. Si fikira za binadamu wala mwenendo wake ungemshawishi au kuhitilafiana na Mungu hata chembe; Mungu Asingebadilisha kiholela mpango Wake, wala Asingebadilisha au kuharibu mpango Wake kwa sababu ya mwenendo wa binadamu, hali ambayo ingekuwa ujinga. Nini, basi, kimeandikwa katika Mwanzo 17:21-22? "Lakini nitaliimarisha agano langu na Isaka, ambaye Sara atakuzalia wewe wakati kama huu mwaka ujao. Naye akakoma kuzungumza na yeye, na Mungu akapanda juu kutoka kwa Ibrahimu." Mungu hakutilia maanani hata chembe kile Ibrahimu alichofikiria au kusema. Na sababu ya kutotilia maanani Kwake ni gani? Kutotilia maanani kwake kulikuwa kwa sababu, wakati huo Mungu hakuhitaji kwamba mwanadamu awe mwenye imani kuu au kwamba aweze kuwa na maarifa makuu kuhusu Mungu, au, vilevile, aweze kuelewa kile kilichofanywa na kusemwa na Mungu. Hivyo, hakuhitaji kwamba binadamu aelewe kabisa kile Alichoamua kufanya, au watu Alioamua kuchagua, au kanuni za vitendo Vyake, kwani kimo cha binadamu hakikutosha tu. Wakati huo, Mungu alichukulia kile ambacho Ibrahimu alifanya na vyovyote alivyojiendesha yeye mwenyewe kuwa kawaida. Hakushutumu, au kukemea, lakini alisema tu: "Sara atakuzalia Isaka wakati huu uliopangwa mwaka ujao." Kwa Mungu, baada Yake kuyatangaza maneno haya, suala hili hatimaye lilikuwa kweli hatua kwa hatua; katika macho ya Mungu, kile ambacho kilikuwa kikamilishwe na mpango Wake kilikuwa tayari kimetimizwa. Baada ya kuikamilisha mipangilio ya hayo, Mungu aliondoka. Kile binadamu hufanya au kufikiria, kile binadamu huelewa, mipango ya binadamu—hakuna chochote kati ya hivi vyote kinacho uhusiano wowote na Mungu. Kila kitu hufanyika kulingana na mpango wa Mungu, kikiendana na nyakati na awamu zilizowekwa na Mungu. Hivyo ndivyo kanuni ya kazi ya Mungu inavyoenda. Mungu haingilii kati chochote kile binadamu anafikiria au kujua, ilhali Haachi mpango Wake, wala kuacha kazi Yake kwa sababu binadamu hasadiki wala kuelewa. Kweli hizi hivyo basi zinakamilishwa kulingana na mpango na fikira za Mungu. Hivi ndivyo hasa tunavyoona kwenye Bibilia: Mungu Alisababisha Isaka kuzaliwa wakati ule Aliokuwa amepanga. Je, kweli zinathibitisha kwamba tabia na mwenendo wa binadamu vilizuia kazi ya Mungu? Havikuzuia kazi ya Mungu! Je, imani ndogo ya binadamu kwa Mungu, na dhana zake na fikira kumhusu Mungu viliweza kuathiri kazi ya Mungu? La, havikuathiri! Hata kidogo! Mpango wa usimamizi wa Mungu hauathiriwi na binadamu, suala, au mazingira yoyote. Kila kitu Anachoamua kufanya kitakamilika na kukamilishwa kwa wakati na kulingana na mpango Wake, na kazi Yake haiwezi kutatizwa na binadamu yeyote. Mungu hupuuza vipengele fulani vya ujinga na kutojua kwa binadamu, na hata upinzani na dhana fulani za binadamu Kwake, Akifanya kazi ambayo lazima Afanye bila ya kujali. Hii ni tabia ya Mungu na ni onyesho la kudura Yake.
Chanzo: Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe II (Sehemu ya Kwanza)
Yaliyopendekezwa: Umeme wa Mashariki Hutoka wapi?
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni