Kwa mara nyingine tena Nitatumia njia ya kusimulia hadithi, ambayo ninyi nyote mnaweza kusikiliza mkiwa kimya na kutafakari juu ya kile Ninachokizungumzia. Baada ya kumaliza kusimulia hadithi, nitawauliza maswali kuona mmeelewa kiasi gani. Wahusika wakuu katika hadithi ni mlima mkubwa, kijito kidogo, upepo mkali, na wimbi kubwa.
Hadithi ya 2. Mlima Mkubwa, Kijito Kidogo, Upepo Mkali, na Wimbi Kubwa
Kulikuwa na kijito kidogo kilichotiririka kwa kuzungukazunguka, hatimaye kikawasili chini ya mlima mkubwa.
Mlima ulikuwa unazuia njia ya kijito hiki, hivyo kijito kikauomba mlima kwa sauti yake dhaifu na ndogo, "Tafadhali naomba kupita, umesimama kwenye njia yangu na umenizibia njia yangu kuendelea mbele." Basi mlima ukauliza, "Unakwenda wapi?" Swali ambalo kijito kililijibu, "Ninatafuta makazi yangu." Mlima ukasema, "Sawa, endelea na tiririkia juu yangu!" Lakini kwa sababu kijito kilikuwa dhaifu sana na kichanga sana, hakukuwa na namna kwake kutiririka juu ya mlima mkubwa hivyo, hivyo hakikuwa na uchaguzi bali kuendelea kutiririka chini ya mlima ...
Upepo mkali ukavuma, ukiwa umekusanya mchanga na vumbi kuelekea ambapo mlima ulikuwa umesimama. Upepo ukaungurumia mlima, "Hebu nipite!" Mlima ukauliza, "Unakwenda wapi?" Upepo ukavuma kwa kujibu, "Ninataka kwenda upande ule wa mlima." Mlima ukasema, "Sawa, kama unaweza kupenya katikati yangu, basi unaweza kwenda!" Upepo mkali ukavuma huku na kule, lakini haijalishi ulikuwa mkali kiasi gani, haukuweza kupenya katikati ya mlima. Upepo ukachoka na ukaacha ili upumzike. Hivyo katika upande ule wa mlima ni upepo dhaifu tu ndio ulivuma kwa vipindi, ambao uliwafurahisha watu waliopo kule. Hiyo ilikuwa ni salamu ambayo mlima ulikuwa unaitoa kwa watu ...
Ufukweni mwa bahari, mawimbi tulivu ya bahari yalizunguka taratibu kwenye mwamba. Ghafula, wimbi kubwa likaja na likanguruma kuelekea kwenye mlima. "Pisha!" wimbi kubwa lilipiga kelele. Mlima ukauliza, "Unakwenda wapi?" Wimbi kubwa halikusita, na likaendelea kutapakaa huku likijibu, "Ninapanua eneo langu na ninataka kunyoosha mikono yangu kidogo. Mlima ukasema, Sawa, kama utaweza kupita juu ya kilele changu, nitakupisha njia." Wimbi kubwa likarudi nyuma kidogo, na kisha likavurumiza kuelekea mlimani. Lakini haijalishi lilijaribu kwa nguvu kiasi gani, halikuweza kufika juu ya mlima. Halikuwa na jinsi bali kurudi nyuma taratibu kurudi kule lilipotoka ...
Kwa karne nyingi kijito kidogo kilichururika taratibu kuzunguka chini ya mlima. Kwa kufuata njia ambayo mlima uliifanya, kijito kidogo kilifanikiwa kufika nyumbani; kilijiunga na mto, na kutiririka kwenda baharini. Chini ya uangalizi wa mlima, kijito kidogo hakikuweza kupotea. Kijito kidogo na mlima mkubwa walitumainiana, walizuiana, na kutegemeana.
Kwa karne nyingi, upepo mkali haukuacha tabia yake ya kuvuma kwenye mlima. Upepo mkali ulivumisha kimbunga "ulipoutembelea" mlima kama ulivyofanya kabla. Uliutisha mlima, lakini haukuwahi kupenya katikati ya mlima. Upepo mkali na mlima mkubwa walitumainiana, walizuiliana, na walitegemeana.
Kwa karne nyingi, wimbi kubwa wala halikupumzika, na kamwe halikuacha kupanuka. Lingenguruma na kuvurumiza tena na tena kwenda kwenye mlima, lakini mlima haukuwahi kusogea hata inchi moja. Mlima uliilinda bahari, na kwa namna hii viumbe ndani ya bahari viliongezeka na kustawi. Wimbi kubwa na mlima mkubwa walitumainiana, walizuiliana, na walitegemeana.
Hadithi hii imeishia hapo. Kwanza, mnaweza kuniambia nini kuhusu hadithi hii, maudhui makuu yalikuwa ni nini? Kwanza kulikuwa na mlima, halafu nini? (Kijito kidogo, upepo mkali, na wimbi kubwa.) Nini kilikitokea kijito kidogo na mlima mkubwa katika sehemu ya kwanza? Mnakumbuka? (Kijito kidogo kilikuwa kinatiririka chini ya mlima mkubwa.) Kijito kidogo kutiririka chini ya mlima, ndicho kisa kilichotokea kati yao? Kijito kilikwenda wapi? Kwa nini tuzungumze juu ya mlima mkubwa na kijito kidogo? (Kwa sababu mlima ulikilinda kijito, kijito hakikuweza kupotea. Walitegemeana.) Unaweza kusema kuwa mlima ulikilinda au kukizuia kijito kidogo? (Ulikilinda.) Inawezekana kuwa ulikizuia? Mlima na kijito kidogo vilikuwa pamoja; ulikilinda kijito, na pia ulikuwa ni kizuizi. Mlima ulikilinda kijito ili kiweze kutiririka kwenda mtoni, lakini pia ulikizuia kutiririka kutapakaa kila sehemu ambapo kingeweza kufurika na kuwa majanga kwa watu. Hii ndiyo hoja kuu ya sehemu hii? (Ndiyo.) Ulinzi wa mlima kwa kijito na kufanya kwake kazi kama kizuizi kulilinda makazi ya watu. Kisha unapata kijito kidogo kikiunganika na mto chini ya mlima na baadaye kutiririka kwenda baharini; je, huo si umuhimu wa kijito kidogo? Kijito kilipotiririka kwenda kwenye mto halafu kwenda baharini, kilikuwa kinategemea nini? Hakikuwa kinategemea mlima? Kilikuwa kinategemea ulinzi wa mlima na mlima kufanya kazi kama kizuizi; je, hii ndiyo hoja kuu? (Ndiyo.) Je, mnauona umuhimu wa milima kwa maji katika tukio hili? (Ndiyo.) Je, hiyo ni muhimu? (Ndiyo.) Je, Mungu ana makusudi Yake ya kutengeneza milima mirefu na mifupi? Kuna makusudi, sio? Hii ni sehemu ndogo ya hadithi, na kutoka tu katika kijito kidogo na mlima mkubwa tunaweza kuona thamani na umuhimu wa Mungu kuviumba vitu hivi viwili. Tunaweza pia kuona hekima Yake na makusudi katika jinsi ya kutawala vitu hivi viwili. Sivyo?
Sehemu ya pili ya hadithi inashughulika na nini? (Upepo mkali na mlima mkubwa.) Je, upepo ni kitu kizuri? (Ndiyo.) Sio lazima, kwa kuwa wakati mwingine ikiwa upepo ni mkali sana unaweza kuwa janga. Ungejisikiaje kama ungelazimika kukaa nje kwenye upepo mkali? Inategemea ulikuwa mkali kiasi gani, sio? Kama ukiwa ni upepo mwanana kidogo, au kama ukiwa ni upepo wa kiwango cha 3-4 basi bado ungeweza kuvumilika, angalau mtu anaweza kupata shida kuendelea kuacha macho wazi bila kufumba. Lakini ungeweza kuvumilia kama upepo ungevuma kwa nguvu na kuwa kimbunga? Usingeweza kuvumilia. Hivyo, ni kosa watu kusema kwamba siku zote upepo ni mzuri, au kwamba siku zote ni mbaya kwa sababu inategemeana na upepo ni mkali kiasi gani. Hivyo mlima una matumizi gani hapa? Je, kwa kiasi fulani haufanyi kazi kama kichujio cha upepo? Mlima unachukua upepo mkali na kuutuliza na kuwa nini? (Upepo mwanana.) Watu wengi wanaweza kuugusa na kuuhisi katika mazingira ambamo wanaishi—je, wanachohisi ni upepo mkali au upepo mwanana? (Upepo mwanana.) Je, hili sio kusudi mojawapo la Mungu la kuumba milima? Je, hii siyo nia Yake? Ingekuwaje kwa watu kuishi katika mazingira ambamo upepo mkali unavumisha vipande vya mchanga bila kitu chochote kuuzuia au kuuchuja? Inaweza kuwa kwamba na mchanga na mawe kuvumishwa, watu wasingeweza kusihi katika eneo hilo? Baadhi ya watu wanaweza kupigwa kichwani na mawe yanayoruka, au wengine wangeingiliwa na mchanga machoni mwao na hivyo kutoweza kuona. Watu wangemezwa kwenye hewa au upepo ungevuma kwa nguvu sana kiasi kwamba wasingeweza kusimama. Nyumba zingeharibiwa na kila aina ya majanga yangetokea. Je, upepo mkali una thamani? (Ndiyo.) Ni thamani gani hii? Niliposema kuwa ni mbaya, basi watu wangeweza kuhisi kwamba hauna thamani, lakini hiyo ni sahihi? Je, kubadilika kuwa upepo mwanana hakuna thamani? Watu wanahitaji nini zaidi kunapokuwa na unyevunyevu au kusongwa? Wanahitaji upepo mwanana kuwapepea, kuchangamsha na kusafisha vichwa vyao, kuamsha kufikiria kwao, kurekebisha na kuboresha hali zao za akili. Kwa mfano, nyote mmekaa chumbani kukiwa na watu wengi na hewa sio safi, ni kitu gani mtakihitaji zaidi? (Upepo mwanana.) Katika maeneo ambapo hewa imetibuliwa na imejaa uchafu inaweza kushusha uwezo wa kufikiri wa mtu, kupunguza mzunguko wao wa damu, na kuwafanya vichwa vyao visiwe vyepesi. Hata hivyo, hewa itakuwa safi ikiwa itapata nafasi ya kujongea na kuzunguka na watu watajihisi nafuu zaidi. Ingawa kijito kidogo na upepo mkali vingeweza kuwa janga, alimradi mlima upo utavibadilisha na kuwa vitu ambavyo kwa kweli vinawanufaisha watu; hiyo si kweli?
Sehemu ya tatu ya hadithi inazungumzia nini? (Mlima mkubwa na wimbi kubwa.) Mlima mkubwa na wimbi kubwa. Mandhari hapa ni mlima mkubwa uliopo kando ya bahari ambapo tunauona mlima, mawimbi tulivu ya bahari, na pia wimbi kubwa. Mlima ni nini kwa wimbi hapa? (Mlinzi na kinga.) Ni mlinzi na pia ni kinga. Lengo la kulinda ni kuilinda sehemu hii ya bahari isipotee ili kwamba viumbe vinavyoishi ndani yake viweze kuishi na kustawi. Kama kinga, mlima hulinda maji ya bahari—chanzo hiki cha maji—yasifurike na kusababisha janga, ambalo linaweza kudhuru na kuharibu makazi ya watu. Hivyo tunaweza kusema kwamba mlima ni kinga na mlinzi. Hii inaonyesha hali ya kutegemeana kati ya mlima na kijito, mlima na upepo mkali, na mlima na wimbi kubwa, na jinsi vinavyozuiliana na kutegemeana, ambayo nimezungumzia.
Kuna kanuni na sheria inayoongoza vitu hivi ambavyo Mungu aliviumba kuendelea kuishi. Mnaweza kuona kile ambacho Mungu alifanya kutokana na kile kilichotokea kwenye hadithi? Je, Mungu aliumba ulimwengu na kupuuzia kile kilichotokea baada ya hapo? Je, Alitoa kanuni na kuunda namna ambazo wao hufanya kazi na halafu kuwapuuza baada ya hapo? Je, hicho ndicho kilichotokea? (Hapana.) Ni nini hicho sasa? (Mungu Anadhibiti.) Mungu bado Anadhibiti maji, upepo na mawimbi. Haviachi bila udhibiti na haviachi vidhuru au kuharibu makazi ya watu, na kwa sababu hii watu wanaweza kuendelea kuishi na kustawi katika nchi hii. Kitu kinachomaanisha kwamba Mungu alikwishapanga kanuni kwa ajili ya kuishi Alipofanya mbingu. Mungu Alipotengeneza vitu hivi, Alihakikisha kwamba vingewanufaisha binadamu, na pia Alividhibiti ili kwamba visiwe shida au majanga kwa binadamu. Ikiwa havingesimamiwa na Mungu, je, maji yangetiririka kila mahali? Je, upepo usingevuma kila sehemu? Yanafuata sheria? Ikiwa Mungu hakuvisimamia visingeongozwa na kanuni yoyote, na upepo ungevuma na maji yangeinuka na kutiririka kila sehemu. Ikiwa wimbi kubwa lingekuwa refu kuliko mlima, je, sehemu hiyo ya bahari ingekuwa bado ipo? Bahari isingeweza kuwepo. Ikiwa mlima haungekuwa mrefu kama wimbi, eneo la bahari lisingekuwepo na mlima ungepoteza thamani na umuhimu wake.
Je, unaiona hekima ya Mungu katika visa viwili hivi? (Ndiyo.) Mungu aliumba ulimwengu na ni Bwana wake; Yeye ndiye Anausimamia na Anaukimu huku Akiangalia kila neno na tendo. Pia Anatazama kila pembe ya maisha ya mwanadamu. Hivyo Mungu Aliuumba ulimwengu na umuhimu na thamani ya kila kitu na vile vile kazi yake, asili yake, na kanuni zake kwa ajili ya kuendelea kuishi zinaeleweka vizuri Kwake kama kiganja cha mkono wake. Mungu Aliuumba ulimwengu; unadhani Anapaswa kufanya utafiti juu ya kanuni hizi zinazouongoza ulimwengu? Je, Mungu Anahitajika kusoma maarifa au sayansi ya kibinadamu kufanya utafiti na kuyaelewa? (Hapana.) Je, kuna mtu yeyote miongoni mwa binadamu ambaye ana elimu kubwa na hekima ya kutosha kuelewa mambo yote kama Mungu Anavyoelewa? Hakuna. Sio? Je, kuna mamajusi au wanabiolojia ambao wanaelewa kweli jinsi ambavyo vitu vinaishi na kukua? Je, wanaweza kweli kuelewa thamani ya uwepo wa kila kitu? (Hawawezi.) Kwa nini? Vitu vyote viliumbwa na Mungu, na haijalishi ni kwa kiasi kikubwa au kwa kina kiasi gani binadamu anajifunza maarifa haya, au ni kwa muda mrefu kiasi gani wanajitahidi kujifunza, hawataweza kuelewa siri na makusudi ya uumbaji wa Mungu wa vitu vyote, hiyo si sahihi? (Ndiyo.)
Baada ya kujadili kwa kina hadi sasa, mnahisi kwamba mna uelewa wa juujuu wa maana ya kidokezo cha kirai "Mungu ni Chanzo cha Uhai kwa Vitu Vyote"? (Ndiyo.) Nilijua kwamba Nilipojadili mada hii watu wengi wangefikiri kwa haraka juu ya jinsi Mungu ni kweli na namna ambavyo neno Lake linatukimu, lakini wangeifikiria tu katika kiwango hiki. Baadhi hata wangehisi kwamba Mungu kukimu maisha ya binadamu, kutoa chakula na kinywaji cha kila siku na mahitaji yote ya kila siku haihesabiki kama kumkimu mwanadamu. Je, baadhi ya watu hawahisi namna hii? Je, nia ya Mungu haipo wazi katika jinsi ambavyo aliumba kila kitu ili kwamba binadamu awepo na kuishi kwa kawaida? Mungu anadumisha mazingira ambamo watu wanaishi na anatoa vitu vyote ambavyo binadamu huyu anahitaji. Aidha, Anasimamia na kuwa mtawala juu ya vitu vyote. Haya yote yanamfanya binadamu kuishi kwa kawaida na kustawi kwa kawaida; ni kwa njia hii ndipo Mungu Anavikimu vitu vyote na binadamu. Je, watu hahitaji kutambua na kuelewa mambo haya? Pengine baadhi wanaweza kusema, "Mada hii ipo mbali sana na maarifa yetu juu ya Mungu Mwenyewe wa kweli, na hatutaki kujua hili kwa sababu binadamu hawezi kuishi kwa mkate pekee, lakini badala yake anaishi kwa neno la Mungu." Hili ni sahihi? (Hapana.) Kosa ni lipi hapa? Je, mnaweza kuwa na uelewa kamili juu ya Mungu ikiwa mnaelewa tu vitu ambavyo Mungu amesema? Ikiwa mnakubali tu kazi Yake na hukumu Yake na kuadibu, je, mtakuwa na uelewa kamili juu ya Mungu? Ikiwa mnaelewa sehemu ndogo tu ya tabia ya Mungu, sehemu ndogo ya mamlaka ya Mungu, hiyo inatosha kupata uelewa juu ya Mungu, sio? (Hapana.) Kwa nini? (Imeegemea upande mmoja zaidi, na hivyo maarifa yetu ni tupu. Lakini wakati tunamjua Mungu katika kila kipengele cha kazi ya Mungu, pamoja na vitu kama milima na vijito, maziwa, mbegu, mwanga wa jua, na mvua—vitu ambavyo tunaviona, kuvitazama, na kuvipitia, tunahisi kwamba uelewa wetu unakuwa wa kweli.) Matendo ya Mungu yanaanza na uumbaji Wake wa ulimwengu na yanaendelea leo ambapo matendo yake ni dhahiri muda wote na kila wakati. Ikiwa watu wanaamini kwamba Mungu yupo kwa sababu tu Amewachagua baadhi ya watu ambao kwao Anafanya kazi Yake kuwaokoa watu hao, na kama wanaamini kwamba mambo mengine hayamhusishi Mungu, mamlaka Yake, hadhi Yake, na matendo Yake, je, hiyo inaweza kuchukuliwa kuwa kumfahamu Mungu kweli? Watu ambao wana hayo yanayoitwa maarifa ya Mungu—ambayo yamejikitia katika mtazamo wa upande mmoja kwamba Mungu yupo tu kwenye kundi la watu. Je, haya ni maarifa ya kweli juu ya Mungu? Sio kwamba watu wenye aina hii ya maarifa juu ya Mungu wanakataa uumbaji Wake wa vitu vyote na utawala wao juu Yao? Baadhi ya watu hawatamani kukiri hili, na wanaweza kufikiria: "Sioni utawala wa Mungu juu ya vitu vyote, ni kitu ambacho kipo mbali sana na mimi na sitaki kukielewa. Mungu Anafanya chochote anachotaka na wala hakinihusu. Ninachokiangalia zaidi ni kukubali uongozi wa Mungu na neno Lake na nitafanywa mkamilifu na nitaokolewa na Mungu. Nitazingatia tu mambo haya, lakini sitajaribu kuelewa kitu kingine chochote, au kukiwazia wazo lolote. Kanuni yoyote ambayo Mungu Aliifanya Alipoviumba vitu vyote au chochote ambacho Mungu Anafanya kuvikimu na kumkimu mwanadamu wala hakinihusu." Haya ni mazungumzo ya aina gani? Hii sio fedheha kabisa? Je, kuna mtu yeyote miongoni mwenu anayefikiri hivi? Ninajua kwamba kuna watu wengi sana wanaofikiri namna hii hata kama hamtasema. Aina ya mtu huyu wa kuamini katika maandiko anaweza kutumia kile kinachoitwa msimamo wao wa kiroho katika namna wanavyotazama kila kitu. Wanataka kumwekea Mungu mipaka katika Biblia, kumwekea Mungu mipaka kwa maneno Aliyoyazungumza, na kumwekea Mungu mipaka katika neno lilikoandikwa. Hawatamani kufahamu zaidi kuhusu Mungu na hawataki Mungu Aweke umakini zaidi katika kufanya mambo mengine. Aina hii ya kufikiri ni ya kitoto na ni ya kidini sana. Je, watu wenye mitazamo hii wanaweza kumjua Mungu? Wanaweza kuwa na wakati mgumu kumjua Mungu. Leo nimesimulia hadithi hizi mbili na nimezungumza juu ya vipengele hivi viwili. Baada ya kuzisikia tu na baada ya kukutana nazo tu, unaweza kuhisi kwamba ni za kina au hata ni za kidhahania kidogo na ngumu kutambua na kufahamu. Inaweza kuwa ni vigumu kuzihusianisha na matendo ya Mungu na Mungu Mwenyewe. Hata hivyo, matendo yote ya Mungu na yote Aliyoyafanya miongoni mwa vitu vyote na miongoni mwa binadamu wote yanapaswa kueleweka kwa wazi na kwa usahihi kwa kila mtu na kwa kila mmoja ambaye anatafuta kumjua Mungu. Maarifa haya yatakupatia uthibitisho wa imani katika uwepo wa kweli wa Mungu. Pia yatakupatia maarifa sahihi juu ya hekima ya Mungu, nguvu Zake, na jinsi ambavyo anakimu vitu vyote. Itakufanya uelewe kwa wazi kabisa uwepo wa kweli wa Mungu na kuona kwamba siyo hadithi ya kubuni, na sio kisasili. Hii inakufanya uone kwamba si ya kidhahania, na sio tu nadharia, na kwamba Mungu hakika sio tu riziki ya kiroho, lakini ni kweli yupo. Aidha, inakufanya umfahamu Yeye kama Mungu kwa namna ambayo amekimu vitu vyote na binadamu; Anafanya hivi kwa njia Yake mwenyewe na kulingana na wizani Wake mwenyewe. Hivyo mtu anaweza kusema kwamba ni kwa sababu Mungu Aliumba vitu vyote na Akavipatia kanuni kwamba kwa amri Yake kila kimoja kinafanya kazi zake kilizopangiwa, vinatimiza majukumu yao, na kutimiza jukumu ambalo lilipewa kila kimoja. Vitu vyote vinatimiza jukumu lao kwa ajili ya binadamu, na hufanya hivi katika sehemu, mazingira ambamo watu wanaishi. Ikiwa Mungu hangefanya mambo namna hii na mazingira ya binadamu hayangekuwa jinsi yalivyo, imani ya watu kwa Mungu au wao kumfuata Yeye—hakuna ambacho kingewezekana; yangekuwa tu mazungumzo ya bure, hii sio sahihi?
Hebu tuchukue mtazamo mwingine katika hadithi hii ambayo tumekwishaisikia—mlima mkubwa na kijito kidogo. Mlima una matumizi gani? Viumbe hai vinastawi juu ya mlima hivyo kuna thamani ya uwepo wake kwa wenyewe. Wakati huo huo, mlima unazuia kijito kidogo, unahakikisha kuwa hakitiririki kuelekea mahali popote kinapotaka na hivyo kuleta janga kwa watu. Hii sio sahihi? Uwepo tu wa mlima unaruhusu viumbe hai kama vile miti na majani na mimea yote mingine na wanyama mlimani kustawi huku pia ukiongoza kijito kidogo kinapopaswa kutiririka; mlima unakusanya maji ya kijito na kuyaongoza kiasili kuzunguka chini yake ambapo yanaweza kutiririka kuelekea mtoni na hatimaye baharini. Kanuni zilizopo hapa hazikutengenezwa na asili, badala yake zilipangwa mahususi na Mungu wakati wa uumbaji. Kuhusu mlima mkubwa na upepo mkali, mlima pia unahitaji upepo. Mlima unahitaji upepo ili kupapasa viumbe hai ambao wanaishi juu yake, na wakati huo huo mlima unazuia jinsi ambavyo upepo unaweza kuvuma kwa nguvu ili kwamba usiharibu na kuteketeza. Kanuni hii inashikilia wajibu wa mlima mkubwa, hivyo kanuni hii kuhusiana na wajibu wa mlima ilipata umbo yenyewe? (Hapana.) Badala yake ilitengenezwa na Mungu. Mlima mkubwa una wajibu wake na upepo mkali una wajibu wake pia. Sasa, kuhusu mlima mkubwa na wimbi kubwa, je, bila mlima kuwa pale maji yangepata mwelekeo wake wa kutiririka yenyewe? (Hapana.) Maji pia yangeharibu na kuteketeza. Mlima una thamani yake kama mlima, na bahari ina thamani yake kama bahari. Kwa njia hii, chini ya mazingira haya ambapo yanaweza kuwepo pamoja kwa kawaida na ambapo kila kimoja hakiingiliani na kingine, pia vinadhibitiana; mlima mkubwa unadhibiti bahari ili isiweze kufurika na hivyo unalinda makazi ya watu, na hii pia inaruhusu bahari kulea viumbe hai vinavyokaa ndani yake. Je, hii sura ya nchi ilipata umbo yenyewe? (Hapana.) Pia iliumbwa na Mungu. Tunaona katika taswira hizi kwamba Mungu Alipoiumba dunia, Alijua kabla mahali ambapo mlima ungesimama, mahali ambapo kijito kingetiririka, kutoka katika mwelekeo ambapo upepo mkali ungeanza kuvuma na kuelekea ambapo ungekwenda, vile vile kiwango cha urefu ambao wimbi lingekuwa. Nia na makusudi ya Mungu yamekumbatiwa ndani ya vitu vyote hivi na ni matendo Yake. Sasa, unaweza kuona kwamba matendo ya Mungu yapo katika vitu vyote? (Ndiyo.)
Chanzo: Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee VII Sehemu ya Tatu Mungu ni Chanzo cha Uhai kwa Vitu VyoteI
Makala Yaliyopendekezwa: Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe I Sehemu ya Kwanza
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni